Na Benton Nollo, Bahi
Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Bahi, Dkt. Fatuma Mganga leo tarehe 29 Oktoba, 2020 majira ya saa 03:30 asubuhi amemtangaza mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kenneth Ernest Nollo kuwa mshindi wa kinyang'anyiro cha Ubunge wa Jimbo la Bahi.
Akitangaza matokeo hayo mbele ya waandishi wa habari na wananchi wa Bahi kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi leo, Dkt. Mganga amesema Nollo amepata kura 40,629 sawa na asilimia 98 ya kura halali (42,683) zilizohesabiwa akimshinda mpinzani wake kutoka Chama cha Wananchi – CUF, Godfrey Job Kamwe aliyepata kura 2,054 sawa na asilimia 2 ya kura halali zilizopigwa.
Aidha, Dkt. Mganga amesema katika uchaguzi huo, Wapiga kura walioandikishwa katika Jimbo la Bahi ni 121,169 ambapo idadi halisi ya waliopiga kura ni watu 44,623, kura halali zilikuwa 42,683 na kura zilizokatialiwa ni 1,940.
Kwa matokeo hayo, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Bahi, Dkt. Fatuma Mganga amemtangaza Kenneth Ernest Nollo kuwa mshindi wa kiti cha Ubunge na kumkabidhi cheti cha ushindi.
Baada ya kukabidhiwa cheti cha ushindi mbunge huyo mteule alitoa shukrani zake za dhati kwa wanabahi kwa kumuwezesha kupata ushindi huo mkubwa wa zaidi ya asilimia 98.
Aidha, Nollo ametaja vipaumbele vyake kuwa ni kuboresha huduma za jamii ili wananchi washiriki kikamilifu katika kujiletea maendeleo.
Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Bahi, Dkt. Fatuma Mganga akitangaza matokeo ya ubunge wa jimbo hilo kufuatia uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020 mbele ya waandishi wa habari na wananchi waliojitokeza kushuhudia tukio hilo lililofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi.
Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Bahi, Dkt. Fatuma Mganga (kushoto) akimkabidhi Hati ya Kuchaguliwa Kuwa Mbunge wa Jimbo la Bahi, Kenneth Ernest Nollo (kulia) baada ya kushinda kinyang'anyiro hicho kupitia Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020.
Mbunge Mteule Jimbo la Bahi, Kenneth Ernest Nollo kwa furaha akionesha kwa Waanshishi wa Habari na Wananchi Hati ya Kuchaguliwa Kuwa Mbunge wa Jimbo la Bahi baada ya kushinda kinyang'anyiro hicho kupitia Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020.
Mbunge Mteule wa Jimbo la Bahi kupitia Chama cha Mapinduzi - CCM, Kenneth Ernest Nollo (kulia) akipongezwa na Omary Makomba (kushoto) ambaye ni Wakala wa mgombea aliyeshindwa kinyang'anyiro hicho kupitia Chama cha Wananchi - CUF, Godfrey Job Kamwe (hakuwepo eneo la tukio). Anayeshuhudia katikati ni Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Bahi, Dkt. Fatuma Mganga.
Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Bahi, Dkt. Fatuma Mganga akizungumza mara baada ya kutangaza matokeo ya ubunge wa jimbo hilo kufuatia uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020.
Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda akizungumza mara baada ya tukio la kutangazwa mshindi wa Ubunge Jimbo la Bahi, Kennth Nollo (hayupo pichani). (Picha zote na Benton Nollo).
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa