Benton Nollo na Rosemary Celu (DMC), Bahi
Serikali ya Mkoa wa Dodoma imekusanya shilingi bilioni 2.9 kutoka katika sekta ya madini kwa mwaka wa fedha 2020/2021 ambapo asilimia 90 ya mapato hayo yanatokana na tozo mbalimbali za Serikali zinazolipwa na Wachimbaji Wadogo wa madini mkoani humo.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwaWachimbaji Wadogo wa madini mkoani humo kuhusu namna bora ya uchukuaji wa sampuli za uchunguzi na uchenjuaji wa madini yaliyofanyika katika Mgodi wa Dhahabu wa Nholi uliopo wilayani Bahi tarehe 03 Mei 2021.
Dkt. Mahenge amefafanua kwamba, katika Sekta ya Madini Mkoa wa Dodoma kwa mwaka wa fedha 2020/2021 umepangiwa kukusanya shilingi bilioni 3 ambapo mpaka mwezi Aprili 2021 tayari mkoa huo umekusanya shilingi bilioni 2.9 sawa na asilimia 98 ya lengo.
“Utajiri huu tulionao tunataka uwafaidishwe wananchi wa Tanzania, na ndiyo maana marehemu Baba wa Taifa hakuyavuna kiholela holela, aliyachelewesha ili tuje tuyavune tukiwa na ujuzi wetu…leo kwa kuruhusu wachimbaji wadogo, maana yake kwa asilimia 100 wanaofaidika ni vijana wetu wa Tanzania…na ili mfadike ndiyo maana mafunzo haya leo yanatolewa”. Amesema Dkt. Mahenge.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema kwamba, kwa kuwa mafunzo hayo yatafanyika kwa nadharia na vitendo yatasaidia kwa kiasi kikubwa kuleta matokeo chanya hali ambayo itasaidia kuinua uchumi wao na kuchangia mapato ya Serikali kutokana na tozo mbalimbali zinazotozwa katika sekta ya madini.
Akizungumza awali, Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mwanahamisi Munkunda, amesema kuwa awali Wachimbaji Wadogo katika Mgodi wa Dhahabu wa Nholi walikuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya umeme, maji nabarabara ya kufika mgodini hapo, ambapo kwa sasa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeboresha miundombinu hiyo.
“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, Wilaya ya Bahi pamoja na mambo mengine kwa sasa ndiyo wazalishaji wakubwa wa madini ya dhahabu, …na hawa unaowaona hapa mbele yako ndiyo wazalishaji wenyewe na ndiyo maana kila wanachokiomba kwetu kama Serikali tunakileta mara moja”. Amesema Munkunda na kuongeza;
“Tunakileta kwa haraka kwa sababu tunafahamu wawekezaji hawa hatutakiwi kuwachelewesha na tunawapa thamani kama walivyo wawekezaji wengine wakubwa, hawa ni wawekezaji wetu wa ndani, ndani ya wilaya, kwahiyo tunawapa thamani ile ile kama walivyo wawekezaji wengine wakija wa nje.”
Munkunda ameishukuru Wizara ya Madini kuputia Tume ya Madini kwa kuendesha mafunzo hayo ambayo amesema yatakuwa msaada mkubwa kwa Wachimbaji Wadogo na yatasaidia kuokoa uharibifu mkubwa wa mazingira katika eneo la machimbo.
Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Nchangwa Marwa, amesema lengo la kuandaa mafunzo hayo ni kuongeza ujuzi wa uchimbaji wa madini pamoja na kujua namna ya uchukuaji wa sampuli na uchenjuaji kwa wachimbaji wa madini ili kuboresha mazingira kwa wachimbaji wadogo.
“Suala la utafiti kwenye uchimbaji mdogo, kukosa ujuzi wa utambuzi wa miamba, pamoja na namna ya uchukuaji wa sampuli kupeleka maabara, hata kutafsiri majibu ya maabara, imekuwa ni shida kubwa kwa wachimbaji wadogo. Hali ambayo ilisababisha uchimbaji wao uwe ni wa kubahatisha…Serikali ya Wamu ya Sita imekusudia kuboresha mazingira ya uchimbaji”. Amesema Mhandisi Marwa.
Mhandisi Marwa amesema ili kupata ufanisi na tija, ofisi yake imekubaliana na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) kutoa mafunzo kwa kundi moja moja na mafunzo hayo kwa kuanzia, yanaanza na Wachimbaji wa Madini ya Dhahabu na baadae kumaliza makundi mengine ya uchimbaji.
Naye, Diwani wa Kata ya Mpalanga, Baraka Ndhahani ameishukuru Serikali kwa kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili Wachimbaji Wadogo katika Mgodi wa Dhahabu wa Nholi hasa ujenzi wa barabara na umeme.
Ndahani amesema pamoja na maboresho hayo uongozi katika mgodi huo umejipanga kuanza ujenzi wa Kituo cha Polisi, Zahanati na Shule Shikizi ambapo tayari tripu 10 za mchanga zimeshasombwa na michango inaendelea. Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma papo hapo baada ya kupewa taarifa hiyo naye kupitia ofisi yake alichangia mifuko 100 ya saruji ambayo alielekeza itumike kujenga Kituo cha Polisi mgodini hapo.
Akishukuru kwa niaba ya Wachimbaji Wadogo, Meneja wa Mgodi wa Dhahabu wa Nholi, Kulwa Limbu, amesema kitendo cha Serikali kupeleka huduma ya nishati ya umeme na kuchonga barabara kutoka Kijiji cha Mzogole kuingia mgodini hapo kumeleta faraja na imani kubwa kwa serikali yao kwamba inawajali, inawatambua na inathamini mchango wao katika kuchangia kukuza uchumi wa nchi yao.
Matukio katika Picha:
(Picha zote na Benton Nollo)
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa