Na Benton Nollo, Nondwa
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Dkt. Fatuma Mganga amewataka Viongozi na Wajumbe wa Kamati za Maendeleo za Kata (WDC) katika Halmashauri ya Wilaya ya Bahi kuhakikisha kuwa wanasimamia ipasavyo suala la ukusanyaji wa mapato katika maeneo yao.
Dkt. Mganga amewataka viongozi na wajumbe wa kamati hizo kuwa wazalendo wa kufichua mbinu ovu zinazoweza kusababisha mianya ya upotevu wa mapato ambapo alisema Halmashauri kwa sasa imeshanunua mashine za kielektroniki (POS) 84 za kukusanyia mapato kwa vijiji vyote 59 vya Halmashauri Wilaya ya Bahi. Dkt. Mganga ameyasema hayo kwa nyakati tofauti alipoghudhuria vikao vya Kamati za Maendeleo za Kata ya Chifutuka na Nondwa leo Aprili 02, 2019.
"Itafika wakati tukiona mambo hayaendi na baadhi ya vijiji havifikii malengo tuliyokubaliana basi mgawanyo wa asilimia kutoka Halmashauri kwenda kwenye vijiji utatolewa kulingana na kiwango ambacho kijiji husika wamekusanya kwa mwezi husika". Alisema Dkt. Mganga
Pia, amezihimiza Kamati hizo kuendelea kuwahamasisha wananchi kujiunga na CHF Iliyoboresha ili waweze kupata huduma za Afya bila kikwazo pindi wanapozihitaji katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya katika Mkoa wa Dodoma.
"Ndugu zangu maradhi huja wakati mtu hana kitu kabisa hivyo, ni vema kama viongozi tukaendelea kuwahamasisha wananchi katika maeneo yetu kujiunga na CHF Iliyoboreshwa ili aweze kunufaika na huduma mbalimbali zinazotolewa katika vituo vyetu vya kutolea huduma za afya ambayo gharama yake ni shilingi elfu 30, watu sita kwa kipindi cha mwaka mmoja". Alisema Dkt. Mganga.
Aidha, amewaagiza Wataalam wa Idara ya Afya kusimamia vema suala la ukusanyaji wa mapato ya huduma za papo kwa papo kwa wagonjwa wasiokuwa na kadi za CHF na kuwakumbusha kuweka rekodi za wagonjwa wanaotibiwa kwa NHIF na amewataka wataalam hao katika maeneo ambako hakuna zahanati waweke utaratibu wa kuwafuata wananchi mahali walipo na kuwapatia huduma za tiba huku akitolea mfano wa Kitongoji cha Iwumba Kijiji cha Ikumbulu, Kata ya Chifutuka na mpakani mwa Kijiji cha Nondwa jirani ya Wilaya ya Manyoni mkoani Singida.
Katika sekta ya elimu amezihimiza kamati hizo kuandaa mpango wa kuwahamasisha wananchi kuchangia ujenzi wa madarasa ili kukabiliana na uhaba wa madarasa na kukamilisha maboma ambayo kimsingi kwa Shule ya Sekondari Magaga amepatiwa na Serikali shilingi milioni 25 kwa ajili ya kukamilisha maboma katika Shule ya Sekondari Magaga. Pia, ameipongeza Kamati ya Maendelo ya Kata ya Nondwa kwa kuhamasisha wananchi kuchangia ujenzi wa madarasa mawili na ofisi ya walimu kwa ajili ya maandalizi ya kupata Shule ya Sekondari ya Kata hiyo.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Chifutuka, Nollo Mnzajila amemshukuru Mkurugenzi huyo kwa ziara yake ambayo amesema kuwa imewahamasisha wao kama viongozi kujituma kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na kumuahidi kusimamia suala la ukusanyaji wa mapato katika vyanzo vyote ikiwa ni pamoja na kusimamia agizo la Mkurugenzi la kuhakikisha ifikapo saa 12:00 jioni hakuna gari lilibeba nafaka linasafiri mpaka saa 12:00 asubuhi na yeyote atakayekaidi basi sheria itachukua mkondo wake.
Naye Diwani wa Kata ya Nondwa, Mussa Lumondo amempongeza Mkurugenzi huyo kwa uamuzi wake wa kuzitembelea Kamati za Maendeleo ya Kata katika Wilaya ya Bahi jambo ambalo alisema ni faraja kwa wajumbe wa Kamati lakini pia linaamsha ari ya uwajibikaji na utendaji kazi kwa watumishi katika maeneo husika.
Dkt. Mganga yupo katika ziara ya kuhudhuria vikao vya Kamati za Maendeleo za Kata katika kata 22 za Wilaya ya Bahi kwa lengo la kuhamasisha shughuli za Maendeleo hasa suala la ukusanyaji wa mapato, elimu, afya na kuhimiza wananchi kuhifadhi chakula cha kutosha ili kukabiliana na baa la njaa katika kaya zao kwa kuwa msimu wa mvua haukuwa na mvua za kutosha.
xxxxxxxxx
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashaurinya Wilaya ya Bahi, Dkt. Fatuma Mganga (kulia) akizungumza kwenye kikao cha Kamati ya Maendeleo Kata ya Nondwa (WDC) kilichofanyika katika jengo la Mahakama ya Mwanzo Kijiji cha Nondwa tarehe 02 Aprili, 2019. Katikati ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nondwa, Mussa Lumondo na kushoto ni Katibu wa WDC Kata ya Nondwa ambaye pia ni Mtendaji wa Kata hiyo, Sifian Nyange.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashaurinya Wilaya ya Bahi, Dkt. Fatuma Mganga (katikati) akizungumza kwenye kikao cha Kamati ya Maendeleo Kata ya Chifutuka (WDC) kilichofanyika Shule ya Sekondari Magaga tarehe 02 Aprili, 2019. Kulia ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Chifutuka , Nollo Mnzajila. Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Nondwa ambaye pia ni Diwani wa Kata hiyo, Mussa Lumondo (kulia) akizungumza wakati wa kikao hicho kilichofanyika katika jengo la Mahakama ya Mwanzo , Kijiji cha Nondwa tarehe 02 Aprili, 2019.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Nondwa wakimsikiliza kwa makini Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Dkt. Fatuma Mganga (hayupo pichani) wakati wa kikao cha Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Nondwa kilichofanyika katika jengo la Mahakama ya Mwanzo , Kijiji cha Nondwa tarehe 02 Aprili, 2019. (Picha zote na Benton Nollo).
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa