Na Benton Nollo na Bernard Magawa (DMC) – Bahi
Wananchi wilayani Bahi mkoani Dodoma wamehimizwa kupanda miti ya kutosha katika maeneo yao ili kuwa na mazingira mazuri yatakayowawezesha kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mwanahamisi Munkunda alipokuwa akizindua zoezi la upandaji miti wilayani humo lililofanyika tarehe 20 Januari 2021 katika Shule Shikizi ya Lionii iliyopo kijiji cha Bahi Sokoni Kata ya Bahi, tukio ambalo lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wilayani humo pamoja na wanafunzi.
“Hakikisheni miti hii tuliyoipanda leo inatunzwa na kukua vizuri ili eneo hili liwe na mazingira bora, nanyi wanafunzi nendeni mkawe mabalozi wazuri wa kuwaelimisha wazazi wenu wapande miti ya kutosha katika maeneo mnayoishi.” Amesema Munkunda.
Awali, akitoa taarifa kuhusiana na kampeni ya upandaji miti wilayani humo, Kaimu Afisa Mazingira Wilaya ya Bahi, Herman Manawa amesema Idara ya Mazingira kupitia Kitengo cha Misitu kwa kushirikiana na Ofisi ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania - TFS wamepanda miti 10,000 katika taasisi mbalimbali ikiwemo miti ya kivuli, matunda pamoja na miti ya asili lengo likiwa ni kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
“Zoezi hili ni endelevu, tumeweka mpango mkakati kuwa kila kata ipande miti 50,000 hivyo kwa kata zetu 22 za Wilaya ya Bahi mwaka huu (2021) tutakuwa tumepanda miti 1,100,000 ambapo kimsingi zoezi hili litasimamiwa na walezi wa kata hizo ambao ni Wakuu wa Idara na Vitengo mbalimbali hapa Halmashauri.” Amesema Manawa na kuongeza;
“Pia, tunao mkakati wa kila kaya ipande miti mitano ambayo itasimamiwa na Wenyeviti wa Vitongoji kuhakikisha miti hiyo inatunzwa na kustawi vizuri.”
Zoezi la upandaji miti Wilayani Bahi ni sehemu ya kuunga mkono kampeni za kuufanya Mkoa wa Dodoma kuwa wa kijani.
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa