Benton Nollo
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Ummy Mwalimu amesema Serikali haijapiga marufuku uingizaji na utumiaji wa kemikali aina ya Zebaki na badala yake imewataka waingizaji na wasambazaji kujisajili kwenye maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Ummy ameyasema hayo wakati akizungumza na wachimbaji wadogo wa dhahabu katika Kijiji cha Nholi wilayani Bahi tarehe 05 Machi 2021 alipofanya ziara ya kikazi kukagua shughuli za uhifadhi wa mazingira mgodini hapo.
Waziri Ummy amesema kuwa asilimia 80 ya kila kilo 100 za zebaki zinazoingizwa nchini hutumika katika shughuli za uchenjuaji hivyo, Serikali inawajibika kupunguza matumizi ya kemikali hiyo ifikapo 2025.
“Ndugu zangu napenda kusisitiza zebaki si haramu na si madawa ya kulevya na wala si bangi hivyo wanaoingiza au kusambaza msijifiche, hamtakamatwa. Sisi Ofisi ya Makamu wa Rais na Wizara ya Madini tutashirikiana kwa pamoja kuhakikisha tunapata teknolojia mbadala na rahisi ya kuchenjua dhahabu isiyo na madhara kwa binadamu.” Amesema Waziri Ummy.
Aidha, Waziri huyo amesema ripoti ya Shirika la Afya Duniani – WHO imebainisha kwamba zebaki ni moja ya kemikali hatari zaidi na kuwa inahatarisha afya ya binadamu kwani inaweza kusababisha magonjwa ya saratani na figo pamoja na madhara kwa wanyama na mimea.
Kwa upande mwingine, Waziri Ummy amewataka wachimbaji hao kutunza mazingira yanayowazunguka mgodini hapo kwa kutokata miti ovyo ili kutumia katika shughuli za uchimaji wa madini badala yake wapate vibali vya kuitumia miti hiyo.
Pia, amewataka wachimbaji hao wasiache masimo wazi wakati wanapotafuta maeneo yenye dhahabu na badala yake wayafukie pamoja na na kuhakikisha zebaki haisambai ovyo kwa inaweza kuleta madhara.
Ummy amesema Serikali inawatambua wachimbaji wadogo kwa kuwa wanajipatia kipato kutokana na shughuli hiyo na pia kupitia wao Serikali inapata mapato.
Kadhalika, Waziri Ummy amesisitiza na kuwataka wamiliki wa migodi kuwapatia vifaa kinga (Protective Gears) wafanyakazi wao ili kuwaepusha na madhara ya zebaki na kuahidi kujengwa kwa kituo cha umahiri cha uchimbaji ili wachimbaji wa eneo hilo wajifunze.
Awali, akizungumza Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mwanahamisi Munkunda amesema Serikali ya Wilaya hiyo imesogeza huduma muhimu katika eneo hilo hasa umeme ambao umesaidia kurahisisha utendaji kazi kwani mashine mbalimbali mgodini hapo sasa zinatumia umeme na amemuaomba Waziri Ummy kwamba Kituo cha Umahiri cha Madini kijengwe wilayani Bahi kwa kuwa ndiyo wilaya inayoongoza kwa uzalishaji wa madini mbalimbali mkoani Dodoma.
Naye, Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Nchagwa Marwa amesema katika kipindi cha kuanzia mwezi Julai 2020 hadi Februari 2021 Mgodi wa Nholi umezalisha zaidi ya kilo 47.24 za madini ya dhahabu ambazo zimeuzwa kwa zaidi ya shilingi bilioni 5 na kuipatia Serikali mrabaha wa shilingi milioni 300 huku Halmashauri ya Wilaya ya Bahi ikipata shilingi milioni 17 kama gawio kwa mujibu wa Sheria za Madini hapa nchini.
Awali akitoa taarifa ya shughuli za uchimbaji wa madini mgodini hapo, Meneja wa Mgodi huo, Kulwa Limbu amesema mgodi huo una leseni 100 ambapo kati ya hizo leseni 4 tu zipo hai, mashimo au maduara 100 yenye zaidi ya wachimbaji 500 na kuongeza kuwa changamoto kubwa katika eneo hilo ni kukosekana kwa maji safi na salama kwa matumizi ya wachimbaji hao pamoja na ubovu wa barabara ya kutoka Dodoma mjini kulifikia eneo hilo.
Matukio katika Picha:
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Ummy Mwalimu (kulia) akizungumza na wachimbaji wadogo wa dhahabu katika Kijiji cha Nholi wilayani Bahi alipofanya ziara ya kikazi kukagua shughuli za uhifadhi wa mazingira mgodini hapo tarehe 05 Machi 2021.
Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda (kulia) akizungumza na wachimbaji wadogo wa dhahabu katika Kijiji cha Nholi wilayani Bahi wakati wa ziara ya kikazi iliyofanywa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira (hayupo pichani) kukagua shughuli za uhifadhi wa mazingira mgodini hapo tarehe 05 Machi 2021.
Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Nchagwa Marwa (katikati) akifafanua jambo mbele ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira (wa kwanza kushoto) wakati wa ziara ya kikazi aliyoifanya kukagua shughuli za uhifadhi wa mazingira Mgodi wa Dhahabu wa Nholi tarehe 05 Machi 2021. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda.
Meneja Mgodi wa Dhahabu Nholi, Kulwa Limbu akiwasilisha changamoto wachimbaji wadogo mgodini hapo wakati wa ziara ya kikazi iliyofanywa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira (hayupo pichani) kukagua shughuli za uhifadhi wa mazingira mgodini hapo tarehe 05 Machi 2021.
Baadhi ya wachimbaji wadogo wa dhahabu katika Kijiji cha Nholi wilayani Bahi wakimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Ummy Mwalimu alipofanya ziara ya kikazi kukagua shughuli za uhifadhi wa mazingira mgodini hapo tarehe 05 Machi 2021.
Picha zote juu ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Ummy Mwalimu (mwenye mtandio wa bluu) alipotembelea Mgodi wa Dhahabu Kijiji cha Nholi wilayani Bahi wakati wa ziara ya kikazi kukagua shughuli za uhifadhi wa mazingira mgodini hapo tarehe 05 Machi 2021.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Ummy Mwalimu (mwenye mtandio wa bluu) alipotembelea Mgodi wa Dhahabu Kijiji cha Nholi wilayani Bahi wakati wa ziara ya kikazi kukagua shughuli za uhifadhi wa mazingira mgodini hapo tarehe 05 Machi 2021. Picha za juu ni Waziri Ummy akikagua Mgodi Mdogo wa kuchenjua dhahabu kwa kutumia Cyanide (CIL) unaomilikiwa na Kampuni ya Binslum.
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa