Mwili wa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli utazikwa tarehe 26 Machi 2021 nyumbani kwao Chato mkoani Geita.
Hayo yamesemwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati akilihutubia taifa kupitia vyombo mbalimbali vya habari muda mfupi mara baada ya kuapishwa Ikulu jijini Dar es Salaam mapema leo tarehe 19 Machi 2021.
Rais Samia ameliambia taifa kuwa kesho tarehe 20 Machi 2021 mwili wa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli utatolewa katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo na kupelekwa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Petro Oysterbay jijini Dar es Salaam kwa ajili ya ibada na baadaye utapelekwa Uwanja wa Uhuru kuagwa na viongozi.
Tarehe 21 Machi 2021 wanachi wa Jiji la Dar es Salaam watapata fursa ya kuuaga mwili wa Dkt. Magufuli na baadaye utasafirishwa kuelekea jijini Dodoma.
Rais Samia amesema tarehe 22 Machi 2021 wananchi wa Dodoma wataaga mwili wa Dkt. Magufuli katika Uwanja wa Jamhuri na kisha utapelekwa jijini Mwanza ambapo wananchi wa Mwanza wataaga tarehe 23 Machi 2021 na baadaye mwili huo utasafirishwa kuelekea Chato mkoani Geita.
Tarehe 24 Machi 2021 mwili wa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli utaagwa na wanafamilia pamoja na wananchi wa Chato.
Baada ya ratiba hiyo tarehe 26 Machi 2021 itafanyika ibada ya misa takatifu kumuombea Hayati Dkt. Magufuli katika Kanisa Katoliki Chato ambapo pia shughuli ya maziko itafanyika.
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa