Benton Nollo, Bahi
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula (Mb) amekutana na changamoto nyingi zinazoikabili Halmashauri ya Wilaya ya Bahi hali iliyomsononesha na kushindwa kuwabana Wataalam wa Idara ya Ardhi na Maliasili Wilayani humo.
Akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja wilayani humo kuhamasisha ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kupitia sekta ya ardhi tarehe 23 Januari 2019, Mabula aliikuta Halmashauriya Wilaya ya Bahi ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ufinyu wa bajeti pamoja na uhaba wa vitendea kazi hasa magari.
Hali ambayo imesababisha Halmashauri kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo kama vile suala la ukusanyaji wa mapato ya Serikali yanayotokana na sekta ya ardhi, kuwapelekea hati za madai wadaiwa sugu wa kodi za ardhi, kupima na kupanga viwanja pamoja na kwenda kuwaelimisha wananchi kuhusu matumizi bora ya ardhi.
“Sekta ya ardhi ni Idara nyeti sana ambayo inaweza kuiingizia Serikali Mapato mengi lakini kama haitawezeshwa kufanya kazi ipasavyo kwa kupatiwa rasilimali fedha na vifaa kama magari basi itashindwa kutekeleza majukumu yake na hivyo kuifanya Serikali kukosa mapato kupitia sekta hiyo”. Alisema Mabula.
Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Chedieli Mrutu alimueleza Naibu Waziri Mabula kuwa, Idara yake haijawahi kupatiwa fedha zinazotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri na kutaja kuwa bajeti ya Idara hiyo kwa mwaka ni shilingi milioni 2.5 na kubainisha kuwa wakati mwingine fedha hiyo haipatikani kabisa.
Mrutu alimueleza Naibu Waziri Mabula kuwa Idara hiyo haina gari kabisa ambalo kimsingi lingeiwezesha Idara yake kufanya kazi za ardhi ambazo wakati mwingine wataalamu wanantakiwa kwenda umbali mrefu kuwahudumia wananchi katika masuala ya ardhi.
Kufuatia hali hiyo, Mabula alitaka kufahamu mgao wa fedha za mapato ya ndani kwa Halmashauri hiyo kwa idara na vitengo vyote vya Halmashauri kwani kwa uzoefu katika maeneo mengi aliyopita nchini alisema Idara ya ardhi imekuwa mtoto yatima kwani inatengwa na kupatiwa kiasi kidogo cha fedha ukilinganisha na idara nyingine hali ambayo kwa Halmashauri ya Bahi baada ya kuhoji hakuna tofauti jambo lililomfanya aishiwe nguvu na kusema kuwa kiukweli Halmashauri ya Bahi inahitaji kusaidiwa na kuangaliwa kwa jicho la pekee.
Mabula alisema kiasi cha shilingi milioni mbili na laki tano kilichotengwa kwa ajili ya Idara ya Ardhi na Maliasili kwa mwaka hakiwezi kufanya kitu kwani idara hiyo ina majukumu mengi sana na hali hiyo ndiyo iliyosababisha makusanyo yawe kidogo kwani mpaka Desemba 2018 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi ilikuwa imekusanya shilingi milioni saba ilhali malengo iliyowekewa ni kukusanya shilingi milioni 47.
Aliongeza kuwa kwa hali ilivyo Halmashauri ya Wilaya ya Bahi haiwezi kufikia asilimia hamsini ya malengo ya Serikali. Hivyo, aliiagiza Ofisi ya Kamishna Msaidizi Kanda ya Kati kuona namna ya kuisaidia Idara hiyo angalau iweze kutatua baadhi ya changamoto.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Leo Mavika alisema Halmashauri yake inakabiliwa na changamoto kubwa ya uhaba wa fedha kwani mapato ni kidogo. Aidha, alisema pamoja na kuwepo kwa changamoto hiyo Halmashauri itajitahidi kuhakikisha kuwa kiasi kidogo cha mapato kitakachopatikana kitagawanywa sawa katika Idara na Vitengo vyote huku Idara ya Ardhi na Maliasili ikipewa kipaumbele kutokana na umuhimu wake.
Aidha, Mavika alimuomba Naibu Waziri huyo kama inawezekana kuisaidia Idara hiyo gari kwani kwa sasa Halmashauri ina magari mazima mawili tu jambo ambalo linafanya utendaji wa shughuli za Halmashauri za kila siku kuwa mgumu sana.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda alisema kuwa ili WIlaya yake itoke mahali ilipo inahitaji mikakati madhubuti na msukumo wa kipekee hasa wa vitendea kazi kwani hali hiyo ndiyo inayowakatisha tamaa watumishi kutokana na kushindwwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa kuwepo changamoto hizo.
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa