Na Benton Nollo, Bahi
Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Bahi, Dkt. Fatuma Mganga amesema maandalizi kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu 2020 jimboni humo yamekamilika kwa asilimia 100.
Dkt. Mganga ameyasema hayo leo tarehe 27 Oktoba 2020 wakati wa ugawaji wa vifaa vya uchaguzi kwa Wasimamizi wa Uchaguzi ngazi ya Kata na Vituo vya Kupigia Kura vilivyohifadhiwa katika jingo la Utawala Hospitali ya Wilaya ya Bahi.
“Leo tarehe 27 tupo katika maandalizi ya mwisho mwisho….tumeshakamilisha kila kitu kinachotakiwa kwa ajili ya uchaguzi mkuu kuendeshwa kama ni vifaa, tumeshapata vifaa vyote kwa asilimia mia moja, watendaji wote waliokuwa wanatakiwa katika vituo 388 wameshafundishwa wote na wote leo wapo hapa wakichukua vifaa vyao vya vituo vyao kwa ajili ya kwenda kuendesha uchaguzi huu katika vituo hivyo 388”. Amesema Dkt. Mganga na kuongeza;
“Magari yapo yote kwa kata zote 22 yameshawasili hapa kwa ajili ya kuwapeleka watendaji hawa na vifaa vyote katika vituo husika na hata suala la fedha zimekuja zote kwa asilimia mia moja”.
Dkt. Mganga ametoa rai kwa wananchi wa Jimbo la Bahi kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwani Serikali ameshatekeleza wajibu wake hivyo ni vema wananchi wakajitokeza ili rasilimali zilizotumika zisipotee.
Amesema Jimbo la Bahi halina changamoto yoyote kwa kila kitu kilichoahidiwa kuletwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi – NEC kimeletwa kwa wakati.
Wananchi waliojiandikisha kupiga kura Jimbo la Bahi ni 121,169.
Picha zote hapo juu ni maandalizi kwa ajili ya kusimamia Uchaguzi Mkuu 2020 katika Jimbo la Bahi. (Picha zote na Benton Nollo).
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa