Na Benton Nollo,
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Daniel Kehogo amewataka Waratibu Elimu Kata (MEK) na Walimu Wakuu wote Wilayani humo, kuhakikisha kuwa wanawasimamia vema walimu hususan ufundishaji shuleni kwa kuwatembelea mara kwa mara ikiwa ni pamoja na kujua maendeleo ya wanafunzi ili kuinua kiwango cha ufaulu katika mtihani wa Darasa la Saba wa mwaka 2018.
Kehogo aliyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku moja kwa Waratibu Elimu Kata 22 na Walimu Wakuu 72 kuhusu ujazaji wa madodoso ya Takwimu za Shule za Awali (TSA), Takwimu za Shule za Msingi (TSM) na Takwimu za Elimu ya Watu Wazima (TWM), yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Bahi tarehe 27 Machi 2018.
“Ndugu zangu tukumbuke kuwa katika matokeo ya mtihani wa Darasa la Saba ya mwaka 2017, Halmashauri yetu ilishika nafasi ya tano katika mkoa wa Dodoma. Hivyo, sisi kama viongozi tutambue kuwa tunao wajibu mkubwa sana kuhakikisha kuwa wanafunzi wanafundishwa na kuelewa ipasavyo masomo yao wawapo darasani ili katika mtihani wa Darasa la Saba wa mwaka 2018 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi iwe ya kwanza kimkoa na kitaifa”. Alisema Kehogo.
Kehogo aliwaeleza washiriki kuwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) kupitia Halmashauri, inalo jukumu la kukusanya takwimu za Elimu ya Awali, Msing, Sekondari, Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi ambazo hukusanywa kila mwaka mwezi Machi kwa kutumia Dodoso la Shule au Kituo kinachotoa elimu kwa ngazi husika.
“Takwimu hizi hutumikakutoa taarifa na picha ya hali halisi iliyofikiwa kutokana na viashiria mbalimbali vya kielimu katika Sekta ya Elimu Msingi na Elimu ya Sekondari Kidato cha Tano na Sita ambavyo huonesha ni kwa kiasi gani utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo imefanikiwa”. Alifafanua Kehogo na kuongeza;
“Ili kufikia lengo hilo la ukusanyaji wa taarifa hizo muhimu kwa usahihi, mafunzo haya yameandaliwa ili kuwawezesha wanaohusika kuelewa kwa ufasaha maswali na takwimu zinazohitajika ili kufanikisha zoezi lengwa na ni muhimu kusoma maelekezo kwa makini kabla ya kuanza ujazaji wa Dodoso”.
Awali akimkaribisha Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Wilaya, Afisa Elimu Msingi, Mohammed Msongo, amewasihi Waratibu Elimu Kata na Walimu Wakuu kufanya kazi kwa ushirikiano na walimu kwani wao kama viongozi wanawajibu wa kutambua na kutatua changamoto zinazowakabili walimu hata kabla ya walimu wanaowaongoza kuwapelekea.
“Tafadhali ndugu zangu tatueni changamoto za walimu katika maeneo yenu. Kiongozi mzuri na mahiri ni yule mwenye uwezo wa kujua changamoto za wale anaowaongoza hata kabla ya wahusika kumueleza”. Alisema Msongo na kuongeza;
“Hakikisheni ninyi kama viongozi mnachapa kazi ili kuleta tija katika sekta ya elimu na ikumbukwe kuwa kipimo kwamba tunafanya kazi ni pale yanapotoka matokeo ya wanafunzi katika mitihani ya Taifa”.
Usahihi wa takwimu za Elimu Msingi ni miongoni mwa vipengele vinavyopimwa katika utoaji wa fedha za Ruzuku ya “Elimu Lipa kwa Matokeo – EP4R” ambazo hutolewa kila mwaka na Serikali kwa lengo la kuboresha miundombinu ya shule, ikama ya walimu, ufuatiliaji wa taaluma shuleni pamoja na uboreshaji wa Mfumo wa Ukusanyaji wa Takwimu za Elimu Msingi (BEMIS) ambapo kupitia Mpango wa EP4R Halmashauri ya Wilaya ya Bahi kwa mwaka wa fedha 2017/2018 ilipatiwa shilingi 187,287,311.00.
Fedha hizo zilipangwa kutekeleza shughuli zifuatazo; Ufuatiliaji, Takwimu, Usimamizi na Tathmini shilingi 18,728,628.00 sawa na 10%, Ikama ya Walimu (Elimu Msingi) shilingi 37,457,257.46 sawa na 20%, Ujenzi wa Madarasa shilingi 74,914,514.92 sawa na 40% na Umaliziaji Maabara shilingi 56,185,886.19 sawa na 30%.
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa