Na Benton Nollo, Bahi
Watahiniwa 3,355 wanatarajiwa kufanya Mitihani ya kumaliza Elimu ya Msingi mwaka 2020 katika Halmashauri ya Wilaya ya Bahi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Dkt. Fatuma Mganga ameyasema hayo ofisini kwake mapema leo tarehe 06 Oktoba 2020 na kwamba maandalizi yote yanayotakiwa kisheria yameshakamilika.
Dkt. Mganga amesema kwamba katika watahiniwa 3,355 wanaotarajiwa kufanya Mtihani huo Wavulani ni 1,520 sawa na asilimia 45 na Wasichana ni 1,835 sawa na asilimia 55 ya watahiniwa wote na tayari maandalizi ya msingi hususan usafiri wa kusambazaji mitihani pamoja na wasimamizi yamekamilika katika vituo vyote 72.
“Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Baraza la Mitihani la Tanzania – NECTA, mtihani huo utaanza siku ya Jumatano tarehe 7 mwezi Oktoba, 2020 kuanzia saa 2.00 asubuhi kwa watahiniwa wote kufanya masomo ya Kiswahili , Hisabati na Sayansi na kukamilika siku ya Alhamisi tarehe 08 Oktoba, 2020 ambapo Watahiniwa hao watafanya masomo ya Lugha ya Kiingereza na Maarifa ya Jamii”. Amesema Dkt. Mganga.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya Wanafunzi katika masomo, Dkt. Mganga amesema kwamba Wanafunzi wote wameendaliwa vizuri kimasomo ambapo mada zote zilifundishwa vizuri na kukamilishwa, na wamefanya majaribio ya kutosha pamoja na Mitihani mbalimbali ya ngazi ya Kata, Wilaya ukiwemo na Mtihani wa MOCK Mkoa, pia wamejengwa vizuri kisaikolojia na Walimu pamoja na Wazazi na kubainisha kuwa Watahiniwa wote wapo vizuri kwa ajili ya kufanya Mitihani huo.
Amewataka Watahiniwa hao kufanya mtihani huo katika hali ya utulivu na kutambua kwamba Mtihani huo wa Taifa ni sawa na Mitihani mingine na pia, amewatakia afya njema wakati wote na kuwaombea kwa Mungu awasaidie.
Pamoja na hayo, Dkt. Mganga amewataka wasimamizi wote kusimamia vizuri mtihani huo kulingana na maelekezo na taratibu zilizotolewa na Baraza la Mitihani la Tanzania kupitia semina waliyopewa na hasa kujiepusha na vitendo vya udanganyifu kwani vitasababisha wanafunzi kufutiwa matokeo yao.
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa